| 20.03.2010 | 02:00 UTC
Majadiliano ya amani ya Mashariki ya Kati kuanza upya hivi karibuni
MOSCOW:
Majadiliano ya amani kati ya Israel na Wapalestina yaliyokwama, huenda yakaanza upya hivi karibuni. Hiyo ni kwa mujibu wa wapatanishi wa kimataifa waliokutana siku ya Ijumaa mjini Moscow, Urusi.
Wajumbe wa Marekani,Umoja wa Mataifa,Umoja wa Ulaya na Urusi - maarufu kama kundi la pande nne- walikutana kujadili mapendekezo mapya kwa azma ya kuwarejesha Wapalestina na Waisraeli katika meza ya majadiliano.
Mjumbe maalum katika Mashariki ya Kati, Tony Blair amesema ni matumaini yake kuwa karibuni utapatikana mpango utakaoanzisha majadiliano yasio ya uso kwa uso. Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amewahimiza Waisraeli na Wapalestina kutekeleza wajibu wao katika jitahada za kutafuta amani.






